KUKUA KWA TEKNOLOJIA YA
HABARI NA MAWASILIANO
Kukua kwa teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) si tu kumerahisisha upatikanaji wa taarifa, bali pia kumechangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa demokrasia na uhuru wa maoni duniani kote. Maendeleo hayo Facebook yanayohusisha kuibuka kwa mitandao ya kijamii kama vile, Twitter, Instagram, WhatsApp na mingineyo. Mbalio na uhuru wa maoni, kumesaidia kukuza biashara, elimu huku kwa upande mwingine pia yakiathiri tamaduni mbalimbali. Maendeleo ya Tehama yamepiku utamaduni uliokuwa umezoelekea katika mawasiliano kama vile uandishi wa barua, magazeti, machapisho, badala yake sasa watu wanatumia simu za mkononi na kompyuta kupata taarifa kwa wepesi zaidi.
Licha ya maendeleo mengine, hili na ukuaji wa uhuru wa maoni na demokrasia limeonekana tishio kwa baadhi ya viongozi duniani na katika baadhi ya nchi Serikali katika nyakati fulani zimeamua kufungia mitandao ya intaneti ili kupunguza kasi ya mawasiliano.
Zimbabwe
Hivi karibuni, Serikali ya Zimbabwe ililazimika kufunga intaneti baada ya kutokea maandamano makubwa ya kupinga ongezeko la bei ya mafuta lililotangazwa na Rais Emerson Mnangagwa.
Mbali na hatua hiyo, zaidi ya watu 400 akiwamo Mchungaji Evan Mawarire aliyekuwa mpinzani mkubwa wa Rais mstaafu Robert Mugabe wamekamatwa kutokana na maandamano hayo.
DR Congo
Kufungwa kwa mawasiliano ya intaneti pia kumetokea nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ambapo siku moja baada ya uchaguzi iliompa ushindi Felix Tshsekedi.
Miji iliyoathiriwa na ufungaji huo ni pamoja na mji mkuu wa Kinshasa na miji ya Goma na Lubumbashi.
Kampuni za huduma za intaneti duniani ilituma ujumbe kwa wateja wake kwamba serikali imeamuru kufungwa kwa huduma hiyo, hata hivyo waziri wa mawasiliano nchini humo, Emery Okundji alisema hajui kuhusu hali hiyo.
Hatua hiyo ililaaniwa na kundi la kampeni la mgombea wa upinzani, Martin Fayulu likiishutumu serikali kwa kuamuru kufungwa kwa mtandao ili kusitisha matangazo ya ushindi mkubwa wa mgombea wake.
Licha ya ushindi wa Tshisekedi kupingwa na mpinzani wake wa karibu, Martin Fayulu, Mahakama ya Katiba ya nchi imethibitisha matokeo hayo.
Marekani
Pamoja na Marekani kuonekana kama kinara wa demokrasia duniani, nako kuna ugomvi usioisha kati ya viongozi wa siasa na mitandao ya jamii.
Rais Donald Trump anayeonekana kukosa uvumilivu wa kukosolewa, ameishambulia mitandao ya kijamii ya Google, Facebook na Twitter akisema ina upendeleo ingawa hajafikia hatua ya kuifunga.
Kupitia ukurasa wake wa Twitter, hivi karibuni Trump ameilaumu mitandao hiyo akisema inapendelea Chama cha Democratic huku ikiwafungia akaunti zao wanachama wa Republican, akisema serikali itafuatilia jambo hilo la kibaguzi.
Tanzania
Kama ilivyo kwa Trump, Rais John Magufuli ameshaeleza kukerwa kwake na mitandao ya jamii kwa nyakati tofauti.
Akihutubia wakati wa kupokea ndege mbili aina ya Bombardier katika uwanja wa ndege wa Julius Nyerere Dar es Salaam Septemba 28, 2016, Rais Magufuli alisema anatamani malaika washuke kuifungia mitandao hiyo.
“Mtu mwingine anasema ndege hizo tumezinunua kila ndege dola 61 milioni, wakati mimi najua ndege hii haikufika hata nusu ya hizo hela tulizonunua. Ana-post pale anaandika uongo. Halafu hata akishajua ukweli wake baadaye wala hatubu,” alisema Rais Magufuli.
Aliongeza, “Nilikuwa natamani siku moja malaika washuke waizime hii mitandao yote, ili baada ya mwaka mzima itakapokuja kufunguka wakute sisi tumeshaitengeneza Tanzania yetu mpya,” alisema.
Mbali na hatua hiyo, tayari hatua kadhaa zimechukuliwa ikiwa pamoja na kutungwa kwa sheria ya makosa ya mitandao ya mwaka 2015. Kupitia sheria hiyo, watu mbalimbali wameshitakiwa kutokana na maandishi waliyotuma kwenye mitandao kinyume na sheria hiyo.
Miongoni mwa waathirika ni mtandao wa Jamii Forums uliofikishwa Mahakamani ukidaiwa kukiuka sheria hiyo na kesi bado inaendelea.
Akitoa maoni yake hivi karibuni, Meneja wa Programu wa Baraza la habari Tanzania (MCT), Pili Mtambalike anaiona sheria hiyo kuwa moja ya sheria kandamizi zinazokwaza uhuru wa kujieleza na demokrasia nchini.
“Sheria ya makosa ya Mtandao (Cyber Crimes Act, 2015) imekuwa ikitumika kunyamazisha mawazo mbadala na kuadhibu wanaokosoa serikali,” anasema.
Anaendelea kufafanua kuwa, hata kanuni za maudhui ya mtandao zimekuwa kikwazo kikubwa kwa haki ya kujieleza na kupata taarifa na kwamba zimerudisha nyuma kwa kasi sana uhuru wa kujieleza na upanukaji wa matumizi ya mtandaoni.
“Kumewekwa masharti magumu ya kufungua na kuendesha blogs ikiwa ni pamoja na malipo makubwa, vitisho vya faini kubwa na vifungo virefu,” anafafanua.
Akizungumzia nguvu ya mitandao, Mkurugenzi mtendaji wa Jamii Forums, Maxence Melo anasema mitandao inazidi kukua duniani kote. “Ukuaji huu unawafanya wananchi wengi kuendelea kupata taarifa na habari mbalimbali hivyo kujikuta wakifunguka na kujua mambo mengi ambayo hawakuwa wakiyajua awali,” alisema Melo.
Anaongeza, “Endapo mamlaka (authorities) zitaendelea kupuuza au kukazana na kutunga sheria tu za kubana matumizi ya mitandao tutajikuta tunaendelea kuwa nyuma ya mataifa mengine.”
“Huwezi puuza kundi la watu zaidi ya milioni 25 ya Watanzania wanaotumia mitandao. Mitandao ingawa inakuwa na taarifa zaidi ya habari, endapo habari hizo zitasambaa bila kutolewa ufafanuzi wananchi wataiamini na athari yake ni kubwa,” alisema.
Hivi karibuni Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mtwara ilitupilia mbali shauri la kupinga matumizi ya kanuni za maudhui ya kimtandao.
Kesi hiyo namba 25 ya mwaka 2018 ilifunguliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Muungano wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu wote kwa pamoja walikuwa wanapinga kanuni za maudhui ya kimtandao.